JIUNGE NA CHADEMA UOKOE RASILIMALI ZA TAIFA
KAMA RASILIMALI HAZITAANZA KUWANUFAISHA WANANCHI WA ENEO HUSIKA KATIKA TAIFA KUNA HAATARI YA TAIFA KUINGIA KWENYE VURUGU KAMA ILIVYO KUWA KWA SUDANI KUSINI
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko makubwa katika
Baraza lake la mawaziri, mawaziri na manaibu wapya wamesema
watahakikisha wanafanya kazi kwa maslahi ya Taifa na Watanzania.
Juzi
Rais Kikwete alifanya uteuzi huo kwa kufanya mabadiliko makubwa ya
Baraza lake kwa kuingiza sura 13 mpya huku mawaziri na naibu mawaziri
nane wakitupwa nje ya baraza hilo.
Katika mabadiliko hayo,
amewapandisha naibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha
mawaziri nane na naibu mawaziri sita, huku mawaziri na naibu mawaziri 22
wakibaki katika wizara zao za awali.
Dk Mgimwa
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti na Mwananchi Jumapili Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk
William Mgimwa, alisema uteuzi huo ni jambo la heshima hivyo ni lazima
kujituma na kufanya kazi kwa maslahi ya Watanzania.
Alipoulizwa
jinsi atakavyokabiliana na changamoto ndani ya wizara hiyo ikiwa ni
pamoja na tuhuma zilizomng ‘oa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Mustapha
Mkulo, Dk Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Kalenga alisema kabla ya kufanya
lolote ni lazima kujiridhisha.
"Bungeni tulikuwa tunazungumza
mengi kuhusu wizara hii lakini niseme kwamba ni lazima ufanye tathmini
na ukishajua hali halisi ya tatizo ndio unaweza kuzungumza suluhisho la
tatizo husika ni nini, hakuna kisichowezekana,” alisema Dk Mgimwa
Alisema
atafanya kazi kwa kujituma na uzalendo mkubwa ili kuhakikisha makusanyo
ya fedha yanaongezeka, matumizi ya fedha yanafanyika kama yalivyopangwa
na kuboresha ukusanyaji wa mapato.
Makamba
Kwa upande
wake Naibu Waziri wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano,
January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema moja ya mambo
ya kufanya katika wizara hiyo ni kuitazama upya gharama za mitandao ya
simu, mitandao kutofika maeneo ya vijijini pamoja na huduma hiyo kuwa
bora zaidi.
"Wizara hii inagusa maisha ya kila siku ya Mtanzania
hivyo kuna ulazima wa kutizama gharama za mitandao ya simu ili iendane
na maisha halisi ya mtanzania” alisema Makamba.
Akizungumzia
masuala ya sayansi, Makamba alisema kuwa kuna ulazima wa kutizama upya
msingi wa elimu ya sayansi kuanzia shule ya msingi kwa kushirikiana na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya
wanafunzi wanaosoma somo hilo.
Pia, aligusia mikakati iliyowekwa
awali ya asilimia moja ya pato la taifa kuingizwa katika ufanyaji wa
tafiti mbalimbali na kwamba umefikia wakati wa suala hilo kuanza
kutekelezwa kikamilifu.
"Tunatakiwa kuondoa urasimu wa matumizi
ya teknolojia, hakuna haja ya watumishi wa Serikali na wananchi kupanga
foleni kwa ajili ya kuchukua fomu, huu ni wakati wa fomu kujazwa katika
mitandao tu,” alisema Makamba.
Hata hivyo, Makamba alisema kuwa mambo mengi anayoyaona na kuyazungumza hata bungeni yameshaanza kufanyiwa kazi na wizara hiyo.
Rashid
Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Suleiman Rashid alisema kuwa
kipaumbele katika wizara hiyo ni kuhakikisha huduma zinawafikia
wananchi, tena kwa ubora mkubwa.
"Huduma ya afya inatakiwa
kuwafikia watu wote nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mgonjwa
anasafirishwa eneo moja mpaka jingine kwa usalama” alisema Dk Rashid.
Rashid
ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji alisema kuwa wizara inatakiwa
kushughulikia sera na kutengeneza mipango mizuri ili watumishi wake
wafanye kazi katika mazingira bora kwa faida yao na Watanzania wote.
Tizeba
Naye
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa
alisema kwa kuwa ni msaidizi wa waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison
Mwakyembe, atahakikisha kila jambo analofanya bosi wake linakwenda sawa.
"Namshuruku
sana Rais Kikwete, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kwa kuwa wao ndio
waliopendekeza mimi kuteuliwa kuwa waziri, nitatumia elimu yangu na
uzoefu katika Serikali katika utendaji wangu wa kazi” alisema Dk Tizeba.
Mahenge
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Dk Binilith Mahenge ambaye
ni Mbunge wa Makete, alisema kuwa atazungumza zaidi mara baada ya
kuapishwa.
Masele Akizungumzia kuteuliwa kwake Masele alisema
kwanza atapambana kudhibiti mali ya umma, kuhakikisha udhibiti wa
madini na kupata thamani halisi ya kile kinachozalishwa.
Pia
alisema atashughulikia matatizo ya wachimbaji wadogo ambao wamekuwa
wakinyonywa ili waweze kupata haki zao stahiki na kuinua uchumi wao.
"Niwahakikishie Watanzania kwamba nimepewa nafasi kubwa na nitafanya kazi kwa uadilifu,"alisema Masele.
Aliongeza
kuwa; "Tutahakikisha tunazipitia sheria na kuhakikisha wamiliki wa
migodi wanawasaidia wananchi na kila sehemu ulipo mgodi tutashughulikia
ili wananchi na serikali vyote vinufaike."
Alisema kuna watu
wanapotosha kuhusu elimu yake, lakini ana Shahada ya Sayansi ya Siasa na
Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam(UDSM) ambako alihitimu mwaka 2004.
Pia amewahi kufanya kazi katika benki kabla ya kupata nafasi ya kuwa Meneja Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Simu ya Mkononi ya Tigo.
Mawaziri walioachwa wazungumza
Baadhi
ya Mawaziri waliochwa kwenye baraza la jipya, wameelezea kilicho moyoni
mwao katika kipindi hiki ambacho sasa watahudhuria Bunge kama wabunge
wa kawaida na watapata fursa ya kuibana Serikali kiutendaji.
Mtufatakamba
Aklizungumza
na Mwananchi Jumapili, aliyekuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athuman
Mfutakamba alisema: "Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais (Jakaya Kikwete)
kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri, kwa kipindi chote cha miaka miwili
nimejifunza na nimekumbana na changamoto nyingi.”
Kuhusu baraza
lililosukwa upya, Mfutakamba alisema anampongeza Rais Kikwete kwa kuteua
watu makini na wenye elimu kusimamia Wizara ya Uchukuzi.
Alisema uteuzi wa Dk Harison Mwakyembe kuwa Waziri wa Uchukuzi na Charles Tizeba kuwa naibu wake, umefanywa kwa umakini.
"Nampongeza
(Rais Kikwete) kwa kuteua watu wengine. Ni watu wazuri na nawafahamu;
Dk Mwakyembe amebobea katika sheria na Tizeba ni mhandisi mwenzangu,”
alisema.
Aliongeza: "Naamini hawa wataweza kusukuma gurudumu la Wizara ya Uchukuzi na kutekeleza kikamilifu Ilani ya CCM.”
Ingawa
kwa sasa hana mamlaka kwenye wizara hiyo, lakini alisema yuko tayari
kutoa mchango wake pale ambapo watamhitaji kwa ushauri.
Kuhusu
mkakati wake kwa sasa, Mfutakamba alisema ataingia bungeni akiwa mbunge
wa kawaida na atashirikiana na wenzake katika kuishauri Serikali katika
mambo mbalimbali ili kuwaletea maendeleo Watanzania.
Nundu
Aliyekuwa
Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu alisema asingependelea kuzungumza na
vyombo vya habari kwa sasa kwa sababu yeye sasa siyo waziri bali ni mtu
wa kawaida.
"Samahani sana. Sizungumzi na magazeti. Mimi siyo waziri tena ni mtu 'private' (mtu binafsi)," alisema Nundu na kukata simu.
Mkulo
Aliyekuwa
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo naye alisisitiza kuwa hayuko
tayari kuzungumza kupitia vyombo vya habari kwa sasa.
Hakupenda kutoa sababu za kuwa na msimamo huo baada ya kukata simu iliasiendelee kuhojiwa.
Miongoni
mwa mawaziri wengine ambao waliachwa kwenye baraza hilo ni waliokuwa
Mawaziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami, Afya na Usatawi wa Jamii,
Dk Haji Mpona, Naibu wake, Dk Lucy Nkya, Nishati na Madini, Wiliam
Ngeleja na Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Dk Mponda na Dk Nkya simu zao zilikuwa zimefungwa wakati wengine zilikuwa zinaita kwa muda mrefu bili kupokelewa.
Wabunge wateule watoa neno
Nao
wabunge wateule wamesema ili kuepusha mvutano baina ya Serikali na
jamii viongozi nchini wanatakiwa kuwajibika na kuwa karibu zaidi na
wananchi huku mmoja wao, Profesa Sospeter Muhongo akisita kuzungumza
kuteuliwa kwake kwa sasa na kufafanua kuwa wanasayansi sio wanasiasa.
Wabunge
hao walioteuliwa juzi na Rais Jakaya Kikwete ni Mwenyekiti wa Chama cha
NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Sospeter Muhongo, kada wa CCM, Janet Mbene na Saada Mkuya.
Wakizungumza
na Mwananchi kwa nyakati tofauti, Mbene ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Uchumi ya chama hicho jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Serikali
ya Mtaa wa Masaki alisema yupo tayari kuwatumikia wananchi kwa kuwa ni
mzalendo.
Mbene ambaye aliwahi kuteuliwa na Rais kuwa Mbunge
Februari 2010 alisema viongozi wanatakiwa kuwa karibu na wananchi ikiwa
ni pamoja na kuwashirikisha na kuwasikiliza matatizo yao.
"Tusipofanya
hivyo wananchi wanaweza kuhisi jambo lolote, inawezekana haya
yaliyotokea kwa mawaziri yametokana na mambo kutowekwa wazi na kutolewa
ufafanuzi, wananchi wanatakiwa kupewa ufafanuzi wa masuala mbalimbali,
pia wapewe huduma muhimu malalamiko yatapungua,”alisema Mbene.
Kada
huyo wa CCM ambaye ameteuliwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa
Fedha na Uchumi alisema alisema , ""Ukiwa waziri kazi hufanyi peke yako
unakuwa na wasaidizi, pia wapo wenzako ambao utawakuta na wana,
unapopata fursa kama hizi unatakiwa kutumia ulichonacho kwa ajili ya
wengine”.
Mbene aliwahi kugombea ubunge wa Viti Maalum kupitia
NGO mwaka 2010 lakini alishindwa na Rita Mlaki. Hivi karibuni aliteuliwa
na Kamati Kuu (CC) ya CCM kuwania Ubunge wa Afrika Mashariki lakini
alishindwa baada ya kupata kura chache katika uchaguzi uliofanyika
Bungeni, Dodoma.
Kwa upande wake Mbatia alisema kuwa ameteuliwa
na Rais kuwa mbunge kutokana na chama chake kuwa na siasa za kujenga
hoja, siasa ambazo zinawafanya watanzania kudai haki zao bila vurugu na
kumwaga damu.
Alisema kuwa hajachaguliwa kwa upendeleo wala
kulipa fadhila na kwamba Rais Kikwete amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
"Katiba iko wazi na imeeleza kuwa
Rais anaweza kuteua mtu yoyote bila kujali anatokea chama gani cha
siasa. Katika suala zima la uongozi hakuna mwenye hati miliki ya
kuwaongoza watanzania” alisema Mbatia
Mbatia ambaye Januari 21
mwaka huu akiwa na viongozi wengine wa chama hicho waliitwa Ikulu kutoa
maoni yao kuhusu Katiba mpya alisema tatizo kubwa linaloikabili nchi ni
mfumo wa elimu ambao unasababisha mmonyoko wa maadili, ukosefu wa
uadilifu na uaminifu, wajibikaji wa pamoja na watu kutopenda kufanya
kazi.
"Mfumo huu unawafanya watu kutoiheshimu Katiba na sheria za
nchi jambo ambalo linasababisha kuwepo na pengo kubwa kati ya mwenye
nacho na asiyenacho” alisema Mbatia.
Alisema kwakuwa sio mbunge wa kuchaguliwa, jukumu lake kubwa ni kuwatumikia watanzania wote, chama chake.
Wakati
Mbatia akieleza hayo Profesa, Sospeter Muhongo ambaye siku nne
zilizopita aliteuliwa kuwa mbunge, juzi ameteuliwa tena kuwa Waziri wa
Nishati na Madini juzi, alisita kuzungumzia uteuzi huo na kusema kuwa
wanasayansi sio wazungumzaji kwa kuwa sio wanasiasa.
Profesa huyo
wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa wa heshima ya
Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini aliomba atafutwe
siku nyingine na kuahidi kuwa atazungumza kwa kirefu kuhusu kuteuliwa
kwake.
Huku akizungumza kwa furaha alisema, "Nisamehe kijana
wangu unajua wanasayansi si wazungumzaji sana kwa kuwa sio wanasiasa,
nipe muda kidogo nakuahidi kuwa tutazungumza mengi tu ila kwa sasa nipe muda