SAKATA la Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda kutangaza nia ya
kuwania urais ndani ya Kikao cha Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM, sasa
linaitikisa Chadema baada ya Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la
chama hicho (Bavicha), Joliana Shonza kupingana hadharani na bosi wake,
John Heche. Wakati Heche akiwa tayari ametoa tamko kumshambulia
Shibuda akisema chama hicho hakitaruhusu mgombea wake urais atangaze
nia kwenye vikao vya CCM, Shonza ameibuka na kusema tamko hilo la bosi
wake siyo la Bavicha ila ni lake binafsi. Jana, Shonza akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam, alilikana tamko la Heche wiki
iliyoipita akisema hakuna kikao ambacho baraza hilo lilikaa na kutoa
kauli moja kumjadili Shibuda. Hii ni mara ya tatu kwa Shibuda
kusababisha mgongano ndani ya Chadema. Aliwahi kupinga msimamo wa
kutotambua matokeo ya urais wa Jakaya Kikwete na badala yake, alishiriki
tafrija Ikulu ndogo Chamwino, baada ya mkuu huyo wa nchi kuzindua Bunge
la 10 na pia, aliwahi kupinga msimamo wa chama hicho kukataa posho
bungeni badala yake alitaka ziongezwe hadi Sh500,000 huku akiziita ni,
"ujira wa mwiha” na kuwarushia makombora baadhi ya viongozi wake akisema
ni wabunge wafanyabiashara. Katika sakata hilo la sasa, Shonzi
alisema: "Naomba ifahamike kwamba tamko alilolitoa Heche siyo la
Baraza, bali ni lake kama Heche. Alipokuwa akitoa tamko hilo hakukuwa na
kikao chochote cha Baraza cha viongozi wa kitaifa wala Sekretarieti ya
Baraza la Vijana la Chadema ili kulijadili suala hili kwa kina bali,
alitumia mwamvuli wa vijana kuhalalisha hoja yake.” Shonza alisema
tamko alilolitoa dhidi ya Shibuda liliandaliwa na kuandikwa na Ofisa
Habari wa Chadema Makao Makuu, kitu ambacho ni kinyume na utaratibu na
kanuni za Bavicha. "Bavicha tumejikamilisha kwa maana ya kwamba,
tuna uongozi wetu kamili wa taifa. Tuna ofisi zetu ambazo ni nje ya
ofisi za makao makuu sasa iweje tamko hilo likaandaliwe makao makuu tena
na mtu ambaye hahusiki na Bavicha?” Shonza alisema kama utaratibu
huo alioutumia Heche ungekuwa unatumiwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kufanya uamuzi binafsi
pasipo kuyajadili na sekretarieti ya chama, wasingeweza kufikia matunda
yanayoonekana hivi sasa. Msimamo wa Heche Wakati
Makamu huyo akimrushia makombora bosi wake, jana Heche naye alitoa
tamko akisema: "Natoa taarifa kwa umma kwamba baada ya mashauriano,
Katibu wa Bavicha, Deogratias Siale ameitisha kikao cha sekretariati
taifa Alhamisi, Mei 24, 2012, kwa ajili ya kujadili na kuwasilisha
mapendekezo kwenye vikao halali vya chama kwa ajili ya hatua zaidi.” Aliongeza,
"Wakati huohuo, nimejulishwa kuwa Makamu wangu (Shonza), leo
amezungumza na vyombo vya habari na kukanusha taarifa niliyotoa kwa
niaba ya Bavicha. Itambulike kuwa majukumu na mamlaka ya mwenyekiti na
kiongozi mwingine yeyote wa Baraza yanabainishwa na Kanuni za Baraza
letu kifungu 5.4.1, ambayo mwenyekiti ndiye msemaji mkuu wa Baraza na
pia ndiye kiongozi mkuu wa Baraza katika ngazi husika.” Alisema
kifungu cha 5.4.2 kinabainisha majukumu ya makamu mwenyekiti ambaye
anapaswa kufanya kazi chini ya mwenyekiti na ndiye msaidizi wake. Alisema
Katiba ya chama ambayo ndiyo msingi mama wa shughuli za Baraza katika
kanuni zake kifungu cha 7.7.1, inabainisha kazi za mwenyekiti na pia
anaweza kufanya nini na wakati gani kwa kushauriana na nani. "Kwa
kutumia kifungu hiki, nilipokea ushauri kutoka kwa viongozi mbalimbali
wa Bavicha, akiwemo makamu mwenyekiti na kushauriana na Katibu na kuona
haja ya kutoa kauli na mwongozo wa nini kitafuata kwa niaba ya baraza
kama hatua ya kwanza,” alisema na kuongeza: Bavicha Shinyanga Bavicha
Mkoa wa Shinyanga nalo jana limetoa tamko na kumkosoa Shibuda. Tamko
hilo lililotolewa na Mwenyekiti wake, Nzemo Renatus, lilisema: "Tatizo
letu na Shibuda ni kutoa kauli hii huku katiba ya Chadema na taratibu
zake anazifahamu. Lakini mbaya zaidi anakidhalilisha chama kwa
kutoa kauli nzito katika kikao cha mahasimu wetu wakuu wa kisiasa, CCM
huku akiwa mwanachama wetu. Ni sawa na mvuvi anayetoboa mtumbwi wake
mwenyewe akiwa katikati ya Ziwa au Bahari.” "Kwa niaba ya Bavicha
Mkoa wa Shinyanga, naungana na kauli ya Mwenyekiti wa Bavicha Taifa.
Tunaomba aitishe kamati ya utendaji ya Taifa haraka iwezekanavyo tuweze
kupitisha maazimio ya kauli tatanishi za Mbunge Shibuda.”
|