PAMOJA TUNAWEZA KULINDA TANZANIA
Statistics |
Total online: 1 Guests: 1 Users: 0 |
JIUNGE NA CHADEMA UOKOE RASILIMALI ZA TAIFA
KAMA RASILIMALI HAZITAANZA KUWANUFAISHA WANANCHI WA ENEO HUSIKA KATIKA TAIFA KUNA HAATARI YA TAIFA KUINGIA KWENYE VURUGU KAMA ILIVYO KUWA KWA SUDANI KUSINI
|
Main » 2012 » May » 11 » Utapeli mwingine kwenye uteuzi wa wakuu wa wilaya
10:25 AM Utapeli mwingine kwenye uteuzi wa wakuu wa wilaya |
CHADEMA, NCCR MAGEUZI, CUF WAUNGANA KUUPINGA, MADIWANI TARIME WAMKATAA DC
UTEUZI
wa wakuu wa wilaya uliotangazwa juzi umezua mjadala baada ya watu wa
kada tofauti wakiwemo wasomi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi wa
kawaida, huku wengine wakidai kwamba ni sehemu ya kulipana fadhili pia
mpango maalum wa CCM kupanga safu yake katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Habari
kutoka ndani ya CCM zinadai kuwa baadhi ya makada wanautizama uteuzi
huo kama moja ya hatua za kuumiza kambi mojawapo ndani ya chama hicho,
wakati kikielekea katika uchaguzi wake wa ndani ambao mchakato wake
tayari umeanza.
Hata hivyo, wakati wadau hao wakikosoa uteuzi
huo, CCM kwa upande wake kimepuuza madai hayo na kuwataka wanaodhani
kuna tatizo la kikatiba, kupeleka hoja zao kwenye Tume ya Kukusanya
maoni ya Katiba Mpya, ili yafanyiwe kazi.
Katika uteuzi huo,
ambao Rais alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya zote nchini, wamo
waandishi wa habari, wabunge wa viti maalumu na baadhi ya makada wa CCM
walioangushwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka juzi na wengine walioshindwa na wapinzani.
Wabunge
hao wa zamani ni Ponsiano Nyami, Suleiman Kumchaya, Dk Charles Mlingwa,
Manju Msambya, Omar Kwaangw’, Venance Mwamoto, Benson Mpesya, Daudi
Felix Ntibenda, Ramadhani Maneno, Gulamhusein Kifu na Esterina Kilasi.
Habari
kutoka ofisi ndogo ya CCM Lumumba na zile za makao makuu ya Umoja wa
Vijana wa Chama hicho (UVCCM) jijini Dar es Salaam zinasema baadhi ya
makada walipigwa na butwaa baada ya majina yao kutokuonekana katika
orodha hiyo kwani walikuwa na matumaini makubwa.
"Huwezi kuamini
hapa kwetu leo wengine wanachekelea na wengine wamenuna…..kisa eti ni
U-DC, kuna makundi yameumizwa, kwanza watu wao wameambulia patupu,
lakini hata wengine waliokuwamo kwenye timu ya zamani wametoswa,”alisema
mmoja wa makada wa chama hicho aliyepo CCM Lumumba.
Habari
kutoka Dodoma ambako pia kuna vikao vya Sekretarieti ya CCM zilidai kuwa
baadhi ya makada wameanza kuhofia nafasi zao katika uchaguzi wa ndani
wa chama hicho baada ya wale waliokuwa wakidhaniwa kuwa watawatetea
kuachwa katika uteuzi huo.
Katiba ya CCM inawatambua wakuu wa
wilaya kuwa wajumbe wa Kamati za Siasa za Wilaya, wakati wakuu wa mikoa
ni wajumbe wa kamati za siasa za ngazi hizo.
Kwa kuwa wajumbe hao
ni wateule wa Rais hutizamwa ndani ya chama hicho kama watu muhimu
ambao hulinda maslahi ya mamlaka zilizowateua, hivyo misimamo yao katika
vikao hivyo huwa na nguvu kubwa ya ushawishi wa kimaamuzi.
"Sasa
wewe unadhani kwamba ukiwa unagombea uongozi wowote, halafu ukaona DC
au Mkuu wa Mkoa anakupinga, ujue huo ndio msimamo wa Bwana mkubwa
(Mwenyekiti wa Taifa ambaye pia ni Rais), kwa hiyo kama ulikuwa na mtu
wako akatoswa ujue ndio hivyo mambo huenda yasiwe mazuri,”alisema kada
mwingine aliyezungumza na gazeti hili makao makuu ya CCM mjini Dodoma
jana.
Vyama vya siasa Kwa upande wake vyama vya Chadema, NCCR
– Mageuzi na CUF vilisema kwa nyakati tofauti kuwa havioni umuhimu wa
kuwapo kwa wakuu wa wilaya na kwamba nafasi hizo ni kwa ajili ya kutoa
ulaji kwa wanasiasa walioshindwa ndani ya CCM.
Hata hivyo, Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kwa wale
wasioridhishwa na uwapo wa wakuu wa wilaya wafikishe hoja zao kwenye
Tume ya Marekebisho ya Katiba ili maoni yao yafanyiwe kazi.
Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema kundi hilo la
wateule wa Rais ni mzigo kwa nchi kwa sababu hawana kazi ya kufanya
zaidi ya kuwajibika kisiasa.
"Tunahitaji nini kutoka kwa Mkuu wa
Wilaya, katika kila wilaya kuna madiwani wanaouchaguliwa na wananchi,
wabunge na Meya ama mwenyekiti wa Halmashauri husika, kweli tunahitaji
DC hapo?” alihoji.
Aliongeza, "Pia kuna wakurugenzi wanaofanya
kazi kwa niaba ya Serikali pamoja na watendaji wengine sasa hawa wakuu
wa wilaya kazi zao zipi.”
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo
alisema , "Chadema hatuwezi kupongeza uteuzi huo kwani hatutambui uwepo
wao.”Mnyika alisema kimsingi, kundi hilo la wateule wa Rais halina kazi
ya kufanya zaidi ya ile ya ujumbe katika Kamati za Siasa za Wilaya za
CCM.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza alisema Watanzania
wanatakiwa kufuta vyeo vya Mkuu wa Wilaya katika Katiba Mpya ambayo
mchakato wa kuiandaa umeshaanza.
Alisema wateule hao mpaka sasa
hawajulikani kazi wanayoifanya ni ipi kwa kuwa kila wilaya kuna mbunge,
wenyeviti wa wilaya, meya wa manispaa, wakurugenzi na watendaji wengine
ambao nao wakati mwingine utendaji wao umekuwa ukiibua migogoro.
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema chama chao hakioni umuhimu
wa wakuu wa wilaya na kwamba hawana msaada wowote kwa wananchi bali
wanalinda maslahi ya chama.
"Wakuu wa wilaya ni makada tu wa
chama hivyo ni muhimu wachaguliwe na si kuteuliwa tu na Rais kwa kuwa
wanajipa mamlaka makubwa,"alisema Mtatiro.
Alisema nchi
haihitaji makada wa CCM ambao wameshindwa kwenye ubunge na kushindwa
kazi maeneo mengine wawekwe kwenye nafasi muhimu kama hizo.
"Wanakwenda
kulinda maslahi ya CCM na si kuwasaidia wananchi. Ni bora hizi nafasi
zifutwe au ziwekewe utaratibu wa kupatikana,"alisema Mtatiro.
Wasomi na wanaharakati Mwanaharakati
kutoka kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC), Harold Sungusia
alisema wakuu wa wilaya na mikoa hawana tija yoyote na kwamba kazi
wanazozifanya zinaweza kufanywa na wakurugenzi wa wilaya.
Alisema
uwepo wa wateule hao ni mwendelezo wa fikra za utawala wa kikoloni kwa
kuwa wahusika hawawajibiki kwa wananchi bali kwa Rais aliyewateua.
Mbunge
wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema uteuzi huo wa wakuu wa wilaya
ni maandalizi ya CCM kukabiliana na Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alisema
kitendo cha kuteuliwa kwa wagombea wanne walioshindwa kwenye uchaguzi
wa ubunge katika Uchaguzi Mkuu kupitia CCM kuwa wakuu wa wilaya ndio
inalithibitisha hilo.
"Mkoa wa Kigoma umetoa ma-DC ambao
wameshindwa katika uchaguzi hii ni ishara kuwa CCM inajipanga kukusanya
fedha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015” alisema Kafulila.
Walioteuliwa
kushika nafasi hiyo ambao kwa kipindi tofauti walikuwa wabunge wa Jimbo
la Kigoma Kusini ni Kifu Gullamhussein na Manju Msambya.
Kafulila alisema kuwa Katiba Mpya itafuta kila kitu na hakutakuwa tena na Mkuu wa Wilaya ifikapo 2015.
"Wakuu wa Wilaya kazi yao ni kupokea Mwenge wa Uhuru tu ambao hauna faida kwa Watanzania” alisema Kafulila.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema uteuzi huo umelenga
kuiimarisha CCM kutokana na vijana kupewa nafasi zaidi.
Alisema
hizo ni dalili kwamba CCM wameona nguvu ya upinzani na sasa wameanza
kujiimarisha kwa kuwatumia vijana na wakuu hao wa wilaya.
"Wamehofia
kuwa wanaweza kwenda Chadema ndio maana wameamua kuwapa nafasi vijana,
hiyo ni changamoto ambayo wameifanyia kazi” alisema Dk Bana.
Mbunge
wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema anachoona ukuu wa
wilaya ni maalum kwa makada wa CCM waliokosa mahala pengine pa kwenda ni
mwendelezo wa ufisadi.
Akitolea mfano wa makada wawili wa CCM
(majina tunayo) ambao sasa ni wakuu wa wilaya, Lissu alisema mmoja kati
yao amepewa cheo hicho baada ya chama hicho tawala kumchakachua wakati
wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
"Baada ya uchakachuaji
huo … alijiuzulu. Uteuzi wa jana wa kada huyo ni ushahidi tosha kwamba U
–DC aliopewa ni rushwa ya wazi wazi." Kwa upande wa Wakili
Majura Magafu alisema anatarajia kuona wakuu wa wilaya hao wapya
walioteuliwa hususani waandishi wa habari na wakili, wanatimiza wajibu
wao kwa kufanya kazi kwa haki na udilifu.
"Mchakato huu wa
uteuzi wa wakuu wa wilaya ulifanywa kwa umakini na Rais Kikwete,
walioteuliwa wasichekelee bali wawajibike kwa wananchi ,hatutarajii
kuwa wataondolewa kwa kashfa kama walioondolewa,” alisema Magafu.
Aliwasisitiza
kutimiza wajibu wao, akiwataka wasiwe wabinafsi wafanye kazi kwa
maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla ili wasije kumdhalilisha Rais
na wale waliomshauri kufanya uteuzi huo. Wakili Patrick
Ngayomela aliupongeza uteuzi huo na kuwataka wakuu hao wa wilaya
walioteuliwa kukabiliana na changamoto nyingi zinazoikabili Serikali
kwa sasa, akiwataka wawe mstari wa mbele kupambana na rushwa na ufisadi.
Ngayomela
alisema ili taifa liwe na maendeleo ni lazima watendaji wafanye kazi
kwa ufanisi, uadilifu na wapambane na vitendo vyote vinavyoashiria
kuwepo kwa matukio ya ufisadi na rushwa. Pia aliwataka waihamasishe
jamii kutambua haki zao na kupambana na vitendo hivyo vinavyorudisha
nyuma uchumi na maendeleo ya taifa.
Tarime wamkataa DC Baraza
la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Tarime limemkataa mkuu wa wilaya
hiyo, John Henjewele kwa madai kuwa ameshindwa kusimamia masuala ya ulinzi na usalama hasa mauaji Mgodi wa Nyamongo.
Msimamo
huo umetolewa na madiwani wote 49 bila kujali itikadi za vyama vyao,
hivyo kusababisha kushindwa kufanyika kwa kikao cha baraza lao,
kilichokuwa mahususi kwa ajili ya kujadili taarifa CAG.
Waligoma
kufanya kikao hicho wakitaka awepo kwanza Mkuu wa Mkoa wa Mara, John
Tupa ili waweze kumkabidhi mkuu huyo wa wilaya kwa maelezo kwamba
hawamhitaji wilayani hapo .
Pia walisisitiza kuwa kama hatatolewa, hawatakuwa tayari kufanya vikao vyovyote ama kupokea maagizo ya Serikali kupitia kwake kwa kuwa hawamtaki na anatakiwa kutafutiwa sehemu nyingine za kufanya kazi.
Kauli za madiwani Mwenyekiti
wa Kambi ya upinzani, Ndesi Charles Mbusiro ambaye ni diwani wa kata ya
Turwa (Chadema), alisema azimio hilo ni la madiwani wote.
"Ndani
ya chama chake kama kada wamezungumza wameshindwa kuelewana ina maana
hata vyombo vya usalama havimwambii Rais ukweli sasa wameleta kwenye
baraza ambako ni wawakilishi wa watu tumekubaliana aondoke na hakuna
mjadala na mkuu wa mkoa amearifiwa,”alisema.
Anthony Manga kata
Nyamaraga, (CCM) alisema ndani ya chama wamekwishamwita na kumweleza
udhaifu wake, lakini ameshindwa kubadilika hasa masuala ya ulinzi na
usalama, kuweka vizuizi ambavyo vinawanyanyasa wananchi kwa kuongeza
rushwa .
Miongoni mwa wakuu wa wilaya wapya yumo wakili wa
zamani wa NSSF, Crispin Meela ambaye alisema ameupokea uteuzi huo kwa
furaha, lakini anatambua changamoto zinazoikabili Serikali hususani za
ubadhilifu wa fedha, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka."Kama
mwanasheria katika nafasi hii nataka kuangalia na kujifunza sheria za
tawala za mikoa na Serikali za mitaa zilizopo kama zinakidhi mahitaji
kwa wakati uliopo kwa sababu zinamapungufu katika dhana ya mgawanyo wa
kazi,”alisema Meela.
|
Views: 674 |
Added by: twangaraha
| Rating: 0.0/0 |
|
|
|