KASHFA nyingine imeibuliwa katika Idara ya Uhamiaji.Taarifa mpya
yenye kurasa tano, imewataja vigogo hao saba wakidaiwa kuwa na utajiri
wa kutisha.Taarifa hiyo ambayo tunayo nakala yake, imedai kuwa vigogo
hao wanamiliki mali na mamilioni ya shilingi katika akaunti zao binafsi. Maofisa
saba wametajwa kwa majina na vituo vyao vya kazi ambavyo ni Lindi, Dar
es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na Moshi. Tuhuma
hizo zimekuja wakati Tume Maalumu iliyoundwa kuchunguza tuhuma za
ufisadi na utoaji wa vibali bandia kwa wageni, ikitajwa kuanza kazi
juzi. Hata hivyo, habari kutoka wizarani zinaeleza kuwa timu hiyo
itaanza rasmi kazi zake leo. Habari za uhakika kutoka ndani ya
Uhamiaji, zimedai kuwa baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wamemhoji meneja
wa benki moja kubwa ya Moshi ili kupata ukweli wa madai kuwa kigogo
mmoja wa Uhamiaji mwenye cheo cha Naibu Kamishna (DCI), anamiliki
akaunti ya fedha za kigeni. Kigogo huyo anahusishwa pia na mtandao
wa utoaji vibali bandia kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi mkoani
Kilimanjaro au kufanya kazi za kujitolea. Ripoti hiyo imetaja
taasisi 13, zikiwamo zisizo za kiserikali (NGO), hospitali na hoteli za
kitalii zinazodaiwa wageni wake walipewa vibali bandia. Mbali na
kumhoji meneja huyo, inadaiwa pia walifanya mahojiano na uongozi wa
kiwanda kimoja kinachodaiwa kukutwa na vibali bandia vya wageni 84. Taarifa
hizo zilidai kuwa maofisa wengine waandamizi wa Uhamiaji kutoka Makao
Makuu, Dar es Salaam walitarajiwa kuwasili Moshi juzi kuungana na
wenzao. Baadhi ya maofisa waliotajwa katika ripoti hiyo kwamba
wana utajiri ni wale waliokumbwa na uhamisho katika idara hiyo, Kia
miezi mitatu iliyopita. Katika ripoti hiyo, kigogo mmoja mwenye
cheo cha DCI anadaiwa kukutwa na Sh700 milioni katika akaunti yake,
achilia mbali kumiliki mali za mamilioni. Mbali na maofisa hao
kumiliki mamilioni ya fedha taslimu, pia wanadaiwa ‘kufanya kufuru’ ya
kununua magari ya kifahari, nyumba na viwanja. Ripoti hiyo
inayodaiwa kuandikwa na Maofisa Uhamiaji wazalendo, imepinga hatua ya
kuhamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine, maofisa wanaotuhumiwa
kukutwa na utajiri ambao haulingani na vipato vyao. "Tunataka
ufanyike ukaguzi wa kina wa vibali vyote vilivyotolewa kati ya
2009/2010, 2010/2011 hadi 2012 na taasisi zote zionyeshe nakala za
vibali,” imedai. Pia taarifa hiyo imependekeza wenzao wote
wanaotuhumiwa kuwa na utajiri wa kutisha wachunguzwe na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). "Haikuwa sahihi kuwahamisha na kuishia hapo, walipaswa wapelekwe Takukuru wachunguzwe chanzo cha utajiri wao.” Pia
wametaka kigogo anayemiliki akaunti ya Dola, achunguzwe ili kujua
alikuwa akifanya biashara gani nje ya utumishi wa umma na kama alilipa
kodi kiasi gani. Baadhi ya maofisa Uhamiaji wamependekeza
kusimamishwa kazi kwa kigogo huyo katika kipindi hiki kwa hofu ya
kuingilia na kuvuruga uchunguzi. Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa
Uhamiaji, Magnus Ulungi aliwaambia waandishi wa habari kuwa imeundwa kwa
tume ya kumchunguza kigogo huyo. Hata hivyo, taarifa
zilizopatikana jana zilisema tume hiyo imepanua wigo wa uchunguzi juu ya
kuwapo kwa vibali bandia katika taasisi mbalimbali. Kabla ya
kuhamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, aliyekuwa Waziri
wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Naodha alikaririwa akisema Kilimanjaro
ni moja kati ya mikoa minane inayomtia kichefuchefu nchini. Waziri
huyo alisema baadhi ya watumishi wamekuwa wakijihusisha na mtandao wa
uingiaji wahamiaji haramu nchini pia kutoa vibali bandia kwa wageni. Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alipoulizwa juzi kuhusu
sakata hilo alisema ni vyema Uhamiaji ikapewa nafasi ya kuchunguza suala
hilo kwa kuwa tayari imeshateua tume ya uchunguzi.
"Kamishna
Mkuu wa Uhamiaji tayari amelifanyia kazi jambo hilo kwa uzito
unaostahili. Tuwape nafasi walichunguze si vyema kuanza kuingilia katika
hatua hii ya mwanzo,” alisema.
Wahamiaji haramu Serikali,
bila mafanikio, imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukomesha tatizo la
wahamiaji haramu linalotajwa kuwa chanzo cha utajiri wa baadhi ya vigogo
wa Idara ya Uhamiaji. Miongoni mwa mikakati iliyowahi kutangazwa
na Wizara ya Mambo ya Ndani ni pamoja na idara hiyo kufanya utafiti kwa
kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mzumbe kubaini chanzo cha ongezeko la
wahamiaji haramu nchini. Akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake bungeni
mwaka 2007/2008 , aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo,
Joseph Mungai alisema matokeo ya utafiti huo ni kuisaidia Serikali
kujua chanzo cha tatizo hilo na jinsi ya kupambana nalo kwa ufanisi
zaidi. Hatua nyingine zinazochukuliwa ni pamoja na maofisa
Uhamiaji kushiriki katika vikao mbalimbali kuanzia ngazi ya vijiji, ili
kuwapa wananchi elimu juu ya masuala yanayohusu uraia na jinsi ya
kukabiliana na wahamiaji haramu; Kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya
habari; Kuweka mtandao wa kompyuta katika vituo vyote vya Uhamiaji ili
kuviunganisha na makao makuu.
Pamoja na Serikali kutangaza
mkakati huo miaka mitano iliyopita, wahamiaji haramu limeendelea kuwa
tatizo sugu linalotia doa utendaji wa idara hiyo.
|